Mauaji ya kutisha Kenya, 76 wauawa na kujeruhiwa
![]() |
Watu wasiopungua 41 wameuliwa kwa
umati katika shambulizi la kushitukiza la alfajiri kwenye kijiji kimoja
cha ndani huko Tana Delta nchini Kenya.
Watu wasiojulikana wamekivamia kijiji
cha Kipao huko Tana River Delta alifajiri ya kuamkia leo na kuua kwa
umati makumi ya watu na kujeruhi makumi ya wengine.
Habari kutoka nchini Kenya zinasema kuwa
mauaji hayo yalifanyika saa tisa usiku kuamkia leo na mbali na kuuawa
watu 41 wakiwemo wanawake na watoto wadogo, yamepelekea kujeruhiwa pia
watu wengine 35.
Watu waliojeruhiwa waliwahishwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Malindi ambako wanaendelea kupata matibabu.
Wavamiaji hao waliwacherenga kwa mapanga
na kuwapiga risasi wanavijiji hao wakati wakiwa wamelala na kupelekea
baadhi yao kukimbilia msituni usiku wa manane licha ya kuweko wanyama
wakali.
Mwezi Agosti na Septemba mwaka huu pia
zaidi ya watu 100 waliuliwa katika machafuko kama hayo kwenye eneo hilo
na kuilazimisha serikali kutuma mamia ya askari wake kwenye eneo hilo. 
